Ripoti yaonyesha vijana wengi nchini hawana heshima
Muktasari:
Ripoti ya utafiti wa stadi za maisha na maadili kwa vijana imeonyesha asilimia kubwa ya vijana nchini hawana heshima, hawajitambui na hawana ushirikiano kwenye mambo mbalimbali ya kijamii.
Dar es Salaam. Utafiti uliozinduliwa Leo Januari 26, 2023 na Taasisi ya Regional Education Learning Initiative (Reli) kwa kushirikiana na Taasisi ya Uwezo Tanzania umeonyesha kundi kubwa la vijana nchini hawana Maadili na stadi za maisha.

Ripoti hiyo ya ' Assesment of Life Skills and Values in East Africa' iliyofanyika Julai, 2022 imehusisha vijana kuanzia umri wa miaka 13 hadi 17 katika wilaya 34, kaya 11,802 zikihusika na vijana 14,645 walihusishwa kutoka Tanzania Bara.

Utafiti huo umeonyesha kijana mmoja pekee kati ya 10 ana heshima na kujali maadili katika jamii, ambayo ni sawa na asilimia 12.5 ya vijana wote waliohusika katika utafiti huo.
Vilevile, ripoti imeonyesha kuwepo kwa uelewa mdogo wa vijana kujitambua na kutatua tatizo ambapo asilimia 16.8 pekee wana uwezo huo.

Akizungumzia matokeo ya utafiti huo, Mbunge wa Jimbo la Ubungo na mdau wa Elimu, Profesa Kitila Mkumbo amesema uelewa mdogo wa kutatua matatizo na stadi za maisha unasababishwa na hali ya ubora wa elimu.

"Vijana waliohusika kwenye uchunguzi huu wengi wapo shuleni, napata mshituko kuona Wanafunzi Wana uelewa mdogo wa kutatua matatizo na nalihusisha hili na ubora wa elimu yetu," amesema.

"Tukiwekeza hapa kwenye elimu Bora huko mbele kazi itakuwa rahisi kwenye stadi za maisha Kama kujitambua, kutatua matatizo, ushirikiano na heshima," ameongeza.